BABU WA LOLIONDO ATABIRI"HIVI KARIBUNI TANZANIA ITAKUWA KIOO CHA AFRIKA NA DUNIA"

MCHUNGAJI mstaafu wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapila ‘Babu wa Loliondo’
amesema Mungu ameendelea kujifunua kwake na kumuonesha kuwa Tanzania
itakuwa kioo cha Afrika na baadaye kioo cha dunia. Ametoa kauli hiyo
Septemba 24, mwaka huu mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati
akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani
Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili
kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini Arusha. Mchungaji Mstaafu
Mwaisapila aliyesifika kwa tiba ya kikombe cha dawa, alisema kuna mambo
mengi ambayo yameandikwa kwenye Biblia na hayakutokea Israeli sasa
yatafanyika Samunge. “Mungu ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na
wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee na nimeyaona, kwa hiyo mtarajie
kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku akishangiliwa. Alisema katika
mafunuo aliyopewa na Mungu ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi
watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa
hiyo kuishukuru serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa
kikombe’ ikiwemo mahema, maji na ulinzi. Pamoja na maono hayo aliyopewa
Babu wa Loliondo, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelist
Assemblies of God Tanzania (EAGT), marehemu Moses Kulola alikuwa
akimpiga waziwazi katika mahubiri yake akidai mwenendo wa tiba alizokuwa
akizitoa hazifanani na mafundisho ya Mungu. Kama hiyo haitoshi,
watumishi mbalimbali wa Mungu wamekuwa hawamuamini. Askofu Mkuu wa
Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe na Mchungaji wa
Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ kwa nyakati
tofauti waliwahi kunukuliwa wakisema hawana imani na tiba ya kikombe
iliyokuwa ikitolewa na Babu wa Loliondo