
Steele
alionyeshwa mlango wa kutokea na Moyes pamoja na wasaidizi wengine wa
zamani wa Ferguson, Mike Phelan na kocha wa timu ya kwanza, Rene
Meulensteen.
NI kiburi! Ni jeuri. David Moyes kumbe alikataa ushauri wa kocha aliyepita wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, aliyemtaka aendelee kuwa na watu wake wa benchi la ufundi, lakini yeye akawatimua na kuleta watu wake.
Hali ya Moyes ni mbaya Old Trafford baada ya timu hiyo kupata pointi
saba katika mechi sita na kocha wa zamani wa makipa wa Manchester United
chini ya utawala wa Ferguson, Eric Steele, ametia chumvi kidonda baada
ya kusema kuwa Moyes ni mbishi.
Steele alionyeshwa mlango wa kutokea na Moyes pamoja na wasaidizi
wengine wa zamani wa Ferguson, Mike Phelan na kocha wa timu ya kwanza,
Rene Meulensteen.
Badala yake, aliamua kuwaleta Chris Woods, Steve Round na Jimmy
Lumsden ambao alikuwa nao Everton huku pia akimteua beki wa zamani wa
United na Everton, Phil Neville kuwa mmoja wa wasaidizi wake.
“Aliongea na mimi, Mick na Rene. Nilimwambia kwamba nadhani ulikuwa
uamuzi wa kishujaa. Alisikiliza ushauri wa Ferguson, lakini akataka awe
mtu mwenye uamuzi wake mwenyewe,” alisema Steele.
Steele aliwasili Man United mwaka 2008 baada ya kufanya kazi na
Manchester City kabla ya hapo. Anasifika kwa kumgeuza David De Gea
kuwa mmoja kati ya makipa bora duniani baada ya kuanza Ligi Kuu England
hovyo.
Anasema kwamba anaheshimu uamuzi wa Moyes wa kuachana na wao, lakini
akaongeza kwamba haukuwa uamuzi mzuri kwa maendeleo ya klabu.
“Sikutaka kuondoka. Nilijua kwamba David alikuwa anakuja na nikawa
najiuliza angekuja na nani. Simlaumu kwa alichokifanya, nimekuwa katika
soka kwa muda mrefu sana, lakini inashangaza kidogo,” alisema.
“Umekutana na timu ambayo ilikuwa na msimu mzuri na imeshinda ligi.
David De Gea alikuwa na msimu bora. Inaleta maana kama hautaki kuendelea
kufanya kazi na watu waliokuwapo. Hata hivyo hilo lipo nje ya uwezo
wangu.”
Kipigo cha mabao 2-1 cha Man United kutoka kwa West Brom Jumamosi
katika uwanja wao wa nyumbani, Old Trafford, kinaiacha United ikiwa na
pointi saba katika nafasi ya 12 ikiwa ni pointi nane nyuma ya vinara
Arsenal.